Michuano ya soka kuwania ubingwa wa taji la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA imeingia siku yake ya pili Jumapili hii jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mchuano wa kwanza ni kati ya Somalia na Kilimanjaro Stars kutoka Tanzania bara mchuano utakaopigwa kuanzia saa nane mchana saa za Afrika Mashariki.
Somalia na Tanzania zipo katika kundi la A pamoja na Ethiopia na Rwanda.
Tanzania inakuja katika mchuano huu baada ya kupata kipigo katika michuano ya kufuzu kwenda kucheza kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi baada ya kipigo cha mabao 7 kwa 0 na Algeria.
Kikosi cha Somalia katika siku za hivi karibuni nacho kimeonekana kutotabirika kutokana na kuimarika kwa wachezaji wa nchi hiyo inayokabiliwa na changamoto za kiusalama, ikilinganishwa na miaka iliyopita walipokuwa wanafungwa mabao mengi katika michuano hii.
Baadaye saa kumi jioni pambano maarufu la Migingo kama linavyofahamika kwa muda mrefu litawakutanisha wapinzani wa muda mrefu majirani Uganda na Kenya.
Harambee Stars ya Kenya ambao ni mabingwa watetezi wa taji hili wanaanza michuano hii wakiwa na kazi kubwa ya kutetea taji lao lakini pia kutaka kufuta masaibu yaliyowakumba wiki iliyopita wakati wa safari yao kwenda Cape Verde kucheza mchuano wa kufuzu katika kombe la dunia nchini Urusi walikoondelewa.
Kocha wa sasa wa Kenya Bobby Williams zamani alikuwa anaifunza Uganda na kuisaidia kunyakua mataji kadhaa ya CECAFA.
Uganda nao watakuja katika mchuano huu wakiwa na matumaini makubwa ya kuendeleza ubingwa wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki hasa baada ya kufuzu katika hatua ya makundi kufuzu kombe la dunia.
Michuano hii ilianza siku ya Jumamosi na ilianza vibaya kwa wenyeji Ethiopia waliofungwa na Rwanda bao 1 kwa 0, huku Burundi wakiwashinda Zanzibar pia kwa bao 1 kwa 0.
Siku ya Jumatatu, Sudan Kusini itachuana na Djibouti huku Sudan wakipambana na Malawi ambao ni waalikwa katika mashindano haya.