Timu za taifa za soka za Zanzibar na Sudan Kusini zimepata matokeo mazuri katika michuano yao ya mwisho ya makundi kuwania taji la Afrika Mashariki na Kati CECAFA.
Zanzibar Heroes ambao tayari wameshaondolewa katika michuano hii, walipata ushindi mkubwa wa mabao 3 kwa 1 baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Harambee Stars ya Kenya.
Matokeo hayo yaliwashangaza mashabiki wa Kenya na kumaliza historia ya miaka 35 ya kutofungwa na Zanzibar.
Safu ya beki ya Harambee Stars ilionekana dhaifu huku kipa wa kikosi hicho David Okello akishindwa kuzuia mashuti mazito ya Zanzibar Heroes.
Kwa matokeo haya, Kenya inasalia na alama 4 na mchuano wa mwisho kati ya Uganda na Burundi siku ya Jumamosi utaamua mustakabili wa Stars kuendelea katika michuano hii.
Timu ya taifa ya Sudan Kusini imeweka historia kwa kufuzu katika hatua ya mwondoano baada ya kuifunga Malawi mabao 2 kwa 0.
Sudan nayo iliifunga Djibouti mabao 4 kwa 0.
Matokeo mengine, Rwanda waliwafunga Somalia mabao 3 kwa 0.
Michuano ya kumaliza hatua ya makundi inatamatishwa mwishoni mwa juma na siku ya Jumamosi, Tanzania watacheza na Ethiopia, huku Uganda wakimenyana na Burundi.
Michuano ya robo fainali itaanza kuchezwa siku ya Jumatatu.