Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars, ilianza vizuri michuano ya mwaka huu ya kuwania taji la CECAFA baada ya kuishinda Uganda Cranes mabao 2 kwa 0 katika uwanja wa taifa jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mabao ya Stars yalitiwa kimyani na washambuliaji Jacob Keli katika kipindi cha kwanza huku Michael Olunga akimaliza kazi katika kipindi cha pili cha mchuano huo baada ya kupata pasi safi kutoka kwa mchezaji mwezake Cliffton Miheso.
Jitihada za Uganda Cranes kushambulia na kupata angalau bao la kufutia machozi ziliambulia patupu kutokana na uimara wa mabeki wa Kenya hasa kipa Boniface Oluoch.
Uganda Cranes ambao wameshinda taji hili mara 13 walikuja katika mchuano huu baada ya kufanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi kuendelea kutafuta tiketi ya kucheza fainali ya kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018.
Kocha wa zamani wa Uganda Cranes Mike Mutebi ameimbia soka25east.com kuwa wachezaji wa Uganda walijisahau baada ya kuishinda Togo nyumbani na ugenini.
“Leo tulilemewa katika idara zote, Kenya walitushinda nafikiri ni kwa sababu wachezaji wetu walijisahau baada ya kufuzu hatua ya makundi kucheza kombe la dunia,”.
“Kenya ilitaka kuwaonesha mashabiki wao kuwa wanaweza kupata ushindi baada ya kutofanya vizuri katika michuano ya kufuzu kombe la dunia,” alisema Mutebi.
Kwa matokeo hayo ya Jumapili Kenya inaongoza kundi la B kwa alama 3 nafasi ya pili inashikiliwa na Burundi pia kwa alama 3 huku Uganda na Zanzibar wakiwa hawana alama.
Mapema siku ya Jumapili, Kilimanjaro Stars ya Tanzania bara iliifunga Somalia mabao 4 kwa 0.
Nahodha John Bocco alikuwa wa kwanza kuifungia timu yake bao kupitia mkwaju wa Penalti na baadaye Elias Maguli kuifungia Tanzania mabao 2 kabla ya Bocco kuongeza lingine.
Tanzania wanaongoza kundi la A kwa alama alama 3 sawa na Rwanda ambao waliwashinda wenyeji wa mashindano haya Ethiopia bao 1 kwa 0 siku ya Jumamosi.
Siku ya Jumamosi, Sudan Kusini itachuana na Djibouti kuanzia saa nane mchana huku Malawi wakipambana na Sudan.