Na: Victor Abuso
Michuano ya nusu fainali kuwania ubingwa wa soka baina ya vlabu vya nchi za Afrika Mashariki na Kati CECAFA inachezwa Ijumaa hii katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam nchini Tanzania.
Mchuano wa kwanza unawakutanisha mabingwa kutoka nchini Kenya Gor Mahia dhidi ya wawakilishi wa Sudan Al Khartoum kuanzia saa nane mchana saa za Afrika Mashariki.
Wawakilishi wa Tanzania Azam FC kwa jina marufu wana lambalamba wa Chamazi watamenyana na klabu ya kukusanya mapato ya Uganda KCCA saa kumi jioni.
Gor Mahia walitinga katika hatua hiyo baada ya kuifunga Malakia ya Sudan Kusini mabao 2 kwa 1 katika mchuano wa robo fainali, huku Al Khartoum wakiwachabanga mabingwa wa zamani wa michuano hii APR kutoka Rwanda mabao 4 kwa 0.
Azam FC kwa upande wao walionesha kuwa wamekomaa katika soka la Afrika Mashariki na kati baada ya kuwaangusha ndugu zao wanajangwani Yanga FC mabao 5 kwa 3 kupitia mikwaju ya penalti.
Mchuano wa robo fainali wa vlabu hivyo viwili ulikuwa mgumu na baada ya dakika tisini, ulimalizika sare ya kutofungana huku kila upande ukikosa nafasi za kupata mabao katika muda wa kawaida.
Maelfu ya mashabiki wa Yanga walifika uwanjani kuwashangilia vijana wao lakini wakaondoka kwa huzuni huku mashabiki wa klabu ya Simba ambao ni watani wao wa jadi wakiishangilia Azam kwa nguvu zao zote.
Baadhi ya mashabiki wa Yanga waliangua kilio na wengine kuzirai baada ya kushindwa kufuzu katika hatua ya nusu fainali.
KCCA nayo walionesha kuwa wao ni moto wa kuotea mbali baada ya kuwagaraza Al Shandy ya Sudan mabao 3 kwa 0 katika mchuano mwingine wa robo fainali siku ya Jumatano.
Jumamosi itakuwa siku ya mapumziko, huku fainali ikiwa ni siku ya Jumapili huku mshindi wa makala haya ya 48 ya michuano ya klabu bingwa alimaarufu Kagame akipata kitita cha Dola za Marekani elfu 30, Mshindi wa pili elfu 20 huku mshindi wa tatu akikabidhiwa Dola elfu 10.