Connect with us

Baada ya Yanga kutangaza kujiondoa kwenye michuano ya kuwania taji la klabu bingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati Cecafa limetangaza kuanza mchakato wa kutafuta timu nyingine itakayochukua nafasi ya Yanga.

Yanga ilitangaza kujiondoa kwenye michuano hiyo siku chache baada ya Cecafa kutoa ratiba ya michuano hiyo inayotazamiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni na kukamilika mwezi wa saba.

Sababu za msingi za kujitoa Kagame Cup ni kufanya maandalizi kwa ajili ya michunao ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo watacheza na Gor Mahia FC ya Kenya, Julai 18, 2018 jijini Nairobi

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amenukuliwa na gazeti la kila siku nchini Tanzania, Habari Leo akisema Cecafa inasubiri ujio wa rais wa TFF aliyepo nchini Urusi ili kutangaza timu itakayochukua nafasi ya Yanga.

“TFF ndio wenyeji wa mashindano, Karia akirudi tutajua nani anachukua nafasi ya Yanga,”amesema Musonye.

Yanga ni washindi mara tano wa michuano hiyo na hivyo ni miongoni mwa timu zenye umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mashabiki wa soka nchini Tanzania, wanaona kukosekana kwa Yanga katika michuano hiyo kutapunguza msisimko wa michuano hiyo.

Katika ratiba ya michuano hiyo ya Kagame, Simba na Yanga zimepangwa pamoja kwenye kundi C ambapo kuna timu zingine ambazo ni Dakadaha ya Somalia pamoja na St. George kutoka Ethiopia.

 

 

African journalist with passion of football reporting.Also i love politics

More in East Africa