Na Victor Abuso
Gor Mahia ya Kenya na Al Khartoum ya Sudan imefuzu katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati CECAFA baada ya ushindi katika hatua ya robo fainali siku ya Jumanne katika uwanja wa taifa wa Dar es salaam nchini Tanzania.
Al Khartoum inayofunzwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana Kwesi Apiah, ilipata ushindi mkubwa wa mabao 4 kwa 0 katika mchuano huo.
Bao la ufunguzi la Al Khartoum lilitiwa kimyani na mchezaji Atif Khalid katika dakika 10 ya mchuano huo, huku Amin Ibrahim akifunga bao la pili katika dakika ya 20 na 40 huku Osman Salaheldin akimaliza kazi kwa kuipa ushindi klabu yake bao la tano.
Kocha Appiah amesema kuwa mabao ya mapema yaliisaidia timu yake kuendelea kujiimarisha katika mchuano huo.
Katika mchuano mwingine, mabingwa wa Kenya Gor Mahia walipata ushindi wa mabao 2 kwa 1 dhidhi ya Malakia ya Sudan Kusini.
Gor Mahia ilipata bao lake la ufunguzi kupitia Godfrey Walusimbi katika dakika za mapema za mchuano huo ulionekana mgumu kwa vijana kutoka Kenya katika kipindi cha pili.
Mabingwa hao wa Kenya sasa watacheza na Al Khartoum katika hatua ya nusu fainali.
Siku ya Jumatano, Al Shandy washinda wa pili wa kundi B wanachuana na KCCA ya Uganda waliomaliza wa pili katika kundi C kwa alama 6.
Mchuano unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania ni kati ya Azam na Yanga, mchuano ambao kwa mashabiki wa timu hizi mbili umekuja mapema na ni kama fainali ya mwaka 2013.
Fainali ya michuano hii ya CECAFA itachezwa siku ya Jumapili.