Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayowajumuisha wachezaji wanaocheza soka nyumbani wameanza maandalizi ya kupambana na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mchuano muhimu wa kufuzu katika fainali ya mashindano ya bara Afrika CHAN, yatakoyofanyika mwaka ujao nchini Rwanda.
Mchuano huo utachezwa tarehe 18 mwezi huu wa Oktoba jijini Kinshasa kabla ya ule wa marudiano baadaye mwezi huu jijini Bangui.
Wachezaji wote 26 wa DRC chini ya kocha Florent Ibengé wameanza maandalizi hayo katika uwanja wa Kimataifa wa Tata Raphael jijini Kinshasa.
Wakati maandalizi hayo yakiendelea, Shirikisho la soka FECOFA limeliandikia barua chama cha soka barani Afrika CAF, kutaka mchuano wa marudiano kutochezwa jijini Bangui kwa sababu za kiusalama.
Nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeendelea kukumbwa na machafuko ya kisiasa na hadi sasa viongozi wa soka nchini DRC wanasema hawajui ni lini wageni wao watafika jijini Kinshasa.
Mashindano ya CHAN yalianza mwaka 2009 na hufanyika kila baada ya miaka miwili na Jamhuri ya Kidemokraisia ya Congo walishinda taji la kwanza wakati mashindano ya kwanza yalipofanyika nchini Cote Dvoire.
Mataifa 16 yatashiriki katika michuano hiyo kati ya Januari tarehe 16 hadi tarehe 7 Februari mwaka 2016.