Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Leopard imealikwa kushiriki katika mashindano kati ya timu ya taifa ya Angola na Zambia mwezi Novemba.
Michuano hiyo itachezwa jijini Luanda na kocha wa Leopard Florent Ibengé, amesema timu yake itatumia michuano hiyo kujiandaa kushiriki katika michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaosakata kabumbu barani Afrika CHAN mwaka 2016 nchini Rwanda. Ibenge pia amedokeza kuwa amepokea mwaliko wa mchuano wa kirafiki dhidi ya Bosnia and Herzegovina na baada ya michuano ya Angola, timu ya taifa itapiga kambi mjini Goma Mashariki mwa nchi hiyo. Tayari DRC imefuzu katika michuano hiyo baada ya wapinzani wao Jamhuri ya Afrika ya Kati kujiondoa katika michuano ya kufuzu kutokana na ukosefu wa fedha.
Mashindano ya CHAN yalianza mwaka 2009 na hufanyika kila baada ya miaka miwili na Jamhuri ya Kidemokraisia ya Congo walishinda taji la kwanza wakati mashindano ya kwanza yalipofanyika nchini Cote Dvoire.
Mataifa 16 yatashiriki katika michuano hiyo kati ya Januari tarehe 16 hadi tarehe 7 Februari mwakani.