Mabingwa mwaka 2009 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Guinea, Mali na Ivory Coast zimefuzu katika hatua ya nusu fainali,katika michuano ya soka kuwania ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza nyumbani mashindano yanyoendelea nchini Rwanda.
Leopard ya DRC ndio timu pekee inayowakilisha ukanda wa Afrika ya Kati katika mashindano haya baada ya kuifunga Rwanda mabao 2 kwa 1 katika hatua ya robo fainali Jumamosi iliyopita katika uwanja wa Amahoro.
DRC sasa itapambana na Guinea siku ya Jumatano katia mechi ya kwanza ya nusu fainali katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.
Guinea kutoka Afrika Magharibi iliyoifunga Zambia mabao 5 kwa 4 kupitia mikwaju ya penalti katika robo fainali nyingine mwishoni mwa juma lililopita, baada ya timu zote kutoka sare ya kutofungana katika muda wa kawaida na ule wa ziada.
Mali na Ivory nazo zitapambana katika nusu fainali nyingine siku ya Alhamisi katika uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali.
Ivory Coast ilifuzu baada ya kuifunga Cameroon mabao 3 kwa 0, huku Mali ikiishinda Tunisia mabao 2 kwa 1 mwishoni mwa juma lililopita.
Guinea imeweka historia katika mashindano haya kwa kufika katika hatua ya nusu fainali wakati huu inaposhiriki mara ya kwanza katika mashindano haya.
Huenda fainali ikazikutanisha nchi kutoka ukanda wa Afrika Magharibi, Guinea, Mali na Ivory Coast au DRC kutoka Afrika ya Kati.
Wachambuzi wa soka wanaona kwa Afrika Magharibi kutoa timu tatu katika Afrika Magharibi ni ishara tosha kuwa soka la eneo hilo limeendelea ukilinganisha na maeneo mengine barani Afrika.
Fainali itachezwa katika uwanja wa Amahoro siku ya Jumapili kuanzia saa moja na nusu saa za Afrika ya Kati.