Na Victor Abuso,
Harambee Stars ya Kenya mwishoni mwa juma lililopita ikiwa ugenini nchini Ethiopia ililemewa baada ya kufungwa mabao 2 kwa 0 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza kufuzu katika fainali za kombe la CHAN mwakani nchini Rwanda.
Wenyeji walianza kwa kutikisa nyavu za Harambee Stars kupitia bao la Asechalew Girma katika dakika ya 23 kipindi cha kwanza, kabla ya Gatoch Panom kufunga bao la ushindi kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika 77 ya mchuano huo.
Harambee Stars walipata nafasi ya kufunga bao na kusawazisha dakika 10 kabla ya kumalizika kwa mpambano huo lakini Kevin Kimani alishindwa kufunga mkwaju wa penalti uliokolewa na kipa wa Ethiopia Tarik Getnet.
Mechi ya marudiano itapigwa mwezi ujao wa Julai jijini Nairobi. Mshindi wa mechi hiyo atapambana na Djibouti ama Burundi huku mshindi akifuzu kwenye michuano ya makala ya 4 ya kombe la CHAN itakayoandaliwa nchini Rwanda mwakani.
Katika matokeo mengine ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Uganda waliwashinda Tanzania mabao 3 kwa 0 huku Djibouti na Burundi ikitoka sare ya bao 1 kwa 1.
Matokeo mengine barani Afrika, Morroco 3 Libya 0, Mauritania 2 Sierre Leone 1, Zimbabwe 2, Comoros 0, Lesotho 0 Bostwana 0, Namibia 2 Zambia 1 na Swaziland 2 Angola 2.
Michuano ya marudiano ni mapema mwezi Julai.