Rais wa Shirikisho la soka nchini Zimbabwe Philip Chiyangwa ambaye pia ni rais wa Baraza la soka Kusini mwa Afrika COSAFA amesema mkutano aliopanga kukutana na viongozi wa soka kutoka mataifa hayo tarehe 24 mwezi huu jijini Harare, utaendelea kama ilivyopangwa.
Chiyangwa amewaalika marais wa soka kutoka ukanda wa COSAFA pamoja na rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA Giani Infatinno kuja kusherehekea naye, baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa COSAFA lakini pia kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwake.
Hata hivyo, rais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF Issa Hayatou amemwandikia barua Chiyangwa kumtaka kusitisha mkutano huo kwa madai kuwa unalenga kuangusha soka la bara Afrika na kwenda kinyume na utaratibu wa CAF.
CAF imeonya kuwa, itamchukulia hatua ikiwa atakwenda kinyume na onyo hilo na kuendelea na mkutano huo.
Hata hivyo, Chiyangwa amemjibu Hayatou na kusema kuwa kusherehekea kuchaguliwa kwake na sikukuu yake ya kuzaliwa yaivunji kanuni za CAF na hivyo ataendelea na mkutano huo.
Haya yanakuja wiki moja baada ya viongozi wa COSAFA kuamua kwa kauli moja kumuunga mkono rais wa Shirikisho la soka nchini Madagascar Ahmad Ahmad kuwania urais wa CAF dhidi ya Hayatou ambaye amekuwa akiongoza CAF tangu mwaka 1988.
Wachambuzi wa soka wanasema Hayatou anaonekana kuwa na wasiwasi baada ya Mataifa 14 ya Kusini mwa bara Afrika kuamua kuwa hawatampigia kura.
Hivi karibuni, kumekuwa na wimbi la kutaka mabadiliko katika uongozi wa soka barani Afrika katika siku za hivi karibuni.
Uchaguzi wa rais wa CAF utafanyika mwezi Machi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.