Timu ya taifa ya soka ya Tanzania inashuka dimbani baadaye hivi leo kumenyana na Mauritius katika mchuano wake wa mwisho wa kundi A, kufuzu katika hatua ya robo fainali kuwania taji la COSAFA.
Mechi hii itachezwa katika uwanja wa Moruleng, kuanzia saa 12 jioni saa za Afrika Mashariki.
Tanzania inakwenda katika mchuano huu wa mwisho wa hatua ya makundi ikiwa inaongoza kundi hilo kwa alama nne, baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Malawi na kutofungana dhidi ya Angola katika mchuano wake wa pili.
Ushindi ni muhimu katika mchuano huu ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.
Angola ambayo pia ina alama nne tika kundi hili baada ya kuishinda Mauritius bao 1-0 na kutofungana na Angola, itamenyana na Malawi katka uwanja wa Royal Bafokeng.
Atakayeongoza kundi hili atamenyana na Afrika Kusini katika hatua ya robo fainali siku ya Jumapili.
Katika hatua nyingine, Msumbuji ilipata ushindi wake wa kwanza wa kundi B, baada ya kuishinda Ushelisheli mabao 2-1 Jumatano usiku.
Ushindi huu unaipa matumaini Msumbiji kuwa katika nafasi ya kufuzu katika hatua ya robo fainali ikiwa itaishinda Madagascar na kuomba kuwa Ushelisheli waifunge Zimbabwe, wanaongoza kundi hili kwa alama 4, ikifuatwa na Madagascar ambayo pia ina alama 4.
Madagscar na Zimbabwe zilishindwa kufungana katika mchuano wa pili siku ya Jumatano.
Ratiba ya Ijumaa:-
Msumbiji vs Madagascar
Zimbabwe vs Ushelisheli
Mshindi wa kundi hili atamenyana na Swaziland katika hatua ya robo fainali siku ya Jumapili.