Na Victor Abuso,
Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania Jamal Malinzi amesema amesikitishwa mno na matokeo mabaya ya mchuano wa ufunguzi wa michuano ya COSAFA kuwania taji la mataifa ya Kusini mwa Afrika, kati ya Taifa Stars na Swaziland siku ya Jumatatu.
Kinyume na wengi walivyotarajia, Swaziland waliwachabanga Tanzania bao 1 kwa 0 katika michuano hiyo inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Malinzi amesisitiza kuwa kama kiongozi wa soka na Mtanzania, amehuzunishwa na matokeo hayo lakini akatoa wito kwa Watanzania kuwa watulivu.
Katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wa Twitter alisema, “Katika situation kama hizi za kufungwa knee jerk reaction huwa haitakiwi badala yake ni kuwa watulivu na kutathmini mwenendo wa timu,”.
Aliongeza kuwa, “Hata hivyo niseme tu kuwa i am dissapointed kama Watanzania wote mlivyokuwa dissapointed na matokeo. Tusubiri michezo iliyosalia tuone.
Mbali na suala la matokeo hayo, Malinzi amesema kuwa anajivunia rekodi ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanafuatilia moja kwa moja michuano inayochezwa na timu ya taifa nje na ndani ya nchi.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2013, katika mechi 13 za Kimataifa ambazo Taifa Stars imecheza zimeonesha moja kwa moja kupitia runinga na kutangazwa kupitia redio.
Taifa Stars ambayo imealikwa katika michuano hiyo sasa ina kazi kubwa kesho Jumatano katika mchuano wake dhidi ya Madagascar ili kuwa na matumaini ya kusonga mbele na kufika katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya COSAFA