Na Victor Abuso,
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars imerejea nyumbani siku ya Jumamosi baada ya kuondolewa katika michuano ya COSAFA baina ya mataifa ya Kusini mwa Afrika.
Taifa Stars imerudi nyumbani mikono mitupu baada ya kushindwa katika mechi zao zote za kundi B wakati walipokuwa wanasaka nafasi ya kufuzu katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Vijana hao wa Dar es salaam walimaliza kundi lao bila ya alama yoyote baada ya kufungwa na Swaziland bao 1 kwa 0, Madagascar nao wakawashinda mabao 2 kwa 0 kabla ya Lesotho kumaliza kazi kwa kuwaangusha kwa bao 1 kwa 0 katika mchuano wa mwisho.
Matokeo haya yamewakasirisha mashabiki wa soka nchini Tanzania ambao wanataka Shirikisho la soka nchini humo TFF kuchukua hatua za haraka kunusuru soka katika taifa hilo.
Rais wa Shirikisho la soka nchini humo Jamal Malinzi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa naye hakufurahishwa na matokeo hayo na siku ya Jumatatu atakutana na wanahabari ili kutoa mwelekeo wa Taifa Stars.
Kocha wa Mart Nooij raia wa Uholanzi amesema binafasi ameshangazwa na matokeo hayo na matarajio yake yalikwenda kinyume na alivyotarajia.
“Mpira wa sasa hautazami nani yupo juu katika orodha ya FIFA, tulikuwa na matumaini makubwa ya kufika mbali lakini baada ya dakika 90 za kila mchezo matokeo hayakuwa mazuri kweti.” alisema Nooij baada ya kuwasili jijini Dar es salaam.
Nooij sasa anasema kilicho mbele yake ni kuiandaa Tanzania kumenyana katika michuano ya kufuzu kuelekea michuano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 walikopangwa katika kundi moja na Misri, Chad na Nigeria.