Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Real Madrid nchini Uhispania na raia wa Ureno Cristiano Ronaldo, ndio mchezaji bora wa soka duniani mwaka huu.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 31, alimshinda mpinzani wake Lionell Messi na kunyakua taji hili la Ballon d’Or katika sherehe zilizofanyika siku ya Jumatatu usiku jijini Paris nchini Ufaransa.
Hili ni taji lake la nne. Msimu uliopita, alikuwa kiungo muhimu sana kuisaidia klabu yake kunyakua taji la klabu bingwa barani Ulaya.
Pamoja na hilo, wakati wa michuano ya bara Ulaya, mshambuliaji huyo aliiongoza nchi yake ya Ureno kushinda michuano hiyo iliyofanyika nchini Ufaransa kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Alishinda taji lake la kwanza mwaka 2008, lakini pia akashinda mwaka 2013, 2014 na sasa mwaka 2016 na sasa yuko nyuma kwa taji moja ili kumfikia Lionell Messi ambaye ameshinda mara tano.
“Nimefurahi sana kupata tuzo hii,” alisema Cristiano.
“Sikuwahi kufikiria kuwa ningeshinda taji hili mara nne,”.
“Nawashukuru wachezaji wenzangu na kila mmoja aliyefanikisha mafanikio haya,” aliongeza.
Orodha kamili ya washindi tangu mwaka 2010:-
2010-Lionel Messi (Barcelona)
2011-Lionell Messi (Barcelona)
2012-Lionell Messi (Barcelona)
2013-Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
2014-Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
2015-Lionel Messi (Barcelona)
2016-Cristiano Ronaldo (Real Madrid)