Klabu ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio mabingwa wa taji la ngao ya jamii msimu huu baada ya kuifunga Saint Eloi Lupopo mabao 3 kwa 0 mwishoni mwa wiki iliyopita katika uwanja wa Kimataifa wa Tata Rafael jijini Kinshasa.
Mabao yote matatu ya Vita Club, yalifungwa katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo huku Bayindula Nkongo akifunga mawili huku Jean Marck Makusu akifunga bao lake mapema katika fainali hiyo.
Taji hili siku zote kuwaniwa kati ya mabingwa wa ligi ya taifa na bingwa wa taji la Congo Cup.
Vita Club sasa wanachukua taji hilo waliloshinda mabingwa wa zamani TP Mazembe walionyakua mara mbili mfululizo mwaka 2013 na 2014.
Mchuano huu unaashiria kuanza kwa msimu mpya wa soka nchini DRC.
Shirikisho la soka nchini humo limeshaweka wazi ratiba ya ligi kuu ambayo inatarajiwa kuanza tarehe 18 mwezi Septemba mwaka 2015.