Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imeanza vema michuano ya mataifa bingwa barani Afrika baada ya kuishinda Morocco bao 1-0 katika mchuano muhimu wa kundi C.
Mchuano huo ulipigwa siku ya Jumatatu usiku katika uwanja wa Oyem nchini Gabon.
Bao pekee la Leopard lilitiwa kimyani na mshambuliaji Junior Kabananga katika kipindi cha pili cha mchuano huo.
Licha ya kupata bao hili, Atlas Lions walionekana kutawala mchezo huo na kuwashambulia wapinzani wao hasa katika za lala salama.
Dakika tisa kabla ya kumalizika kwa mchuano huo, DRC ilibaki na wachezaji 10 baada ya Joyce Lomalisa Mutambala kupewa kadi nyekundu kwa kumfanyia madhambi mchezaji wa Morocco.
Hali iligeuka na kuwa mbaya zaidi baada ya mchezaji mwingine wa DRC Gabriel Zakuani kulazimika kuondoka uwanjani baada ya kupata jeraha baya, na kuwaacha vijana wa kocha Florent Ibenge kupambana wakiwa tisa hadi kumalizika kwa mchuano huo.
Kikosi
DR Congo: Matampi; N’Sakala (Lomalisa 65′), Zakuani, Tisserand, Mpeko – Mubele, Mulumba, Bope, Mbemba, Kabananga (Maghoma 72′) – Bakambu (Mbokani 77′)
Morocco:El Kajoui; Mendyl, Da Costa, Benatia, Dirar – El Kaddouri (En Nesyri 61′), Saiss (Fajr 73′), El Ahmadi, Boussoufa, Carcela (El Arabi 79′) – Bouhaddouz
DRC sasa inaongoza kundi la C kwa alama 3 baada ya ushindi huo, ikifuatwa na mabingwa watetezi Ivory Coast na Togo ambazo zina alama moja baada ya kutoka sare ya kutofungana.Morocco ni ya mwisho bila ya alama.
Ratiba ya michuano ijayo:-Januari 20 2017.
- Ivory Coast vs DR Congo
- Morocco vs Togo