Klabu ya Esperance de Tunis ya Tunisia ndio mabingwa wapya wa taji la klabu bingwa barani Afrika, baada ya kuishinda Al Ahly ya Misri, mabao 3-0 katika mzunguko wa pili wa fainali uliyochezwa Ijumaa usiku.
Saad Bguir, ndiye aliyekuwa shujaa wa mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa mjini Rades, kwa kuifungia klabu yake mabao 2.
Hili ni taji la tatu la Esperance katika fainali za klabu bingwa Afrika.
Mbali na Bquir, Anice Badri alifunga bao la tatu, katika mchuano huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa Esperance chini ya ulinzi mkali.
Wachezaji wa Esperance wamesema hawatasahau ushindi huu, na unawaendea mashabiki wa klabu hiyo pamoja na kocha wao wa zamani Khaled Ben Yahia.
Ben Yahia aliondoka katika klabu hiyo, baada ya kufungwa na Primeiro Agosto ya Angola katika mechi ya mzunguko wa kwanza ya nusu fainali na kuacha maswali mengi, iwapo alikuwa amefutwa kazi au kujiuzulu.
Mbali na taji hilo la CAF, Esperance imejishindia Dola za Marekani Milioni 2.5.
Historia ya taji hili:-
Al Ahly ya Misri, imeshinda mataji manane.
TP Mazembe ya DRC, Zamalek ya Misri imeshinda mara tano.
Canon Yaounde ya Cameroon, Esperance (Tunisia), Hafia (Guinea), Raja Casablanca (Morocco) imeshinda mara tatu.
Mara mbili, Asante Kotoko (Ghana), Entente Setif (Algeria, Enyimba (Nigeria), JS Kabylie (Algeria), Wydad Casablanca (Morocco).
Mara moja, ASEC Mimosas, Stade Abidjan (Ivory Coast ), Club Africain, Etoile Sahel (Tunisia), Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates (Afrika Kusini), Oryx Douala, Union Douala (Cameroon), CARA (Congo), FAR Rabat (Morocco), Hearts of Oak (Ghana), Ismaily (Misri), Mouloudia Alger (Algeria), V Club (Congo).