Klabu ya soka ya ES Tunis ya Tunisia na Raja Casablanca ya Morocco, zinamenyana kutafuta ubingwa wa taji la CAF Super Cup.
Huu ni mchuano ambao humkutanisha bingwa wa taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika baada ya kumalizika kwa msimu wa kutafuta ubingwa wa mataji hayo mawili.
Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Thani Bin Jassim mjini Doha, kuanzia saa moja asubuhi saa za Afrika Mashariki.
Mechi hiyo ilikuwa imepangwa kuchezwa mjini Rades nchini Tunisia, mwezi Desemba mwaka 2018 lakini Shirikisho la soka barani Afrika CAF, lilitangaza kuwa mechi hiyo ingechezwa nchini Qatar.
Hii ni mara ya kwanza kwa mechi hii ya Super Cup, kuchezwa nje ya bara la Afrika na iwapo baada ya dakika 90 hakutakuwa na mshindi, hakutakuwa na muda wa ziada, mikwaju ya penalti itapigwa ili kumpata mshindi.
Fainali ya taji hili, inaashiria mabadiliko ya kalenda ya michuano ya klabu bingwa na Shirikisho ambayo itaanza mwezi Agosti na kumalizika mwezi Mei, kutoka mwezi February hadi Novemba.
Fainali ijayo ya taji hili, itachezwa mwezi Agosti, baada ya kumalizika kwa michuano ya mataifa bingwa barani Afrika itakayofanyika mwezi Juni hadi Julai mwaka huu.
Mabingwa watetezi wa taji hili ni Wydad Casablanca ya Morocco.
Al Ahly ya Misri imeshinda taji hili mara sita, huku TP Mazembe na Zamalek wakishinda mara tatu.
Etoile du Sahel na Enyimba ya Nigeria imeshinda mara mbili.