Sakata la ufisadi katika Shirikisho la soka duniani FIFA, lilitikisa ulimwengu wa soka mwaka huu unaomalizika wa 2015.
Mwezi Mei Shirika la ujasusi la Marekani FBI likishirikiana na viongozi wa mashtaka nchini Uswizi liliwatuhumu watu 14 wakiwemo viongozi wa juu wa FIFA kwa kujihusisha na ulaji rushwa.
Miongoni mwa washukiwa hao walikuwa katika Kamati Kuu ya FIFA, Eduardo Li rais wa Shirikisho la soka nchini Costa Rica na Eugenio Figueredo ambaye wakati mmoja alikuwa anaongoza soka nchini Uruaguay.
Maafisa saba walikamatwa katika hoteli ya kifahari ya Baur au Lac mjini Zurich wakati wakijiandaa kushiriki katika kikao cha mkutano Mkuu wa FIFA ambao ulifuatiwa na uchaguzi wa rais wa FIFA.
Jack Warner aliyekuwa wakati mmoja rais wa Shirikisho la soka katika Mataifa ya Marekani na Carrebian CONCACAF na pia kuhudumu katika wadhifa wa Naibu rais wa FIFA naye alitajwa katika sakata hilo na kukanusha kuhusika.
Inadaiwa kuwa maafisa hao waligawana kitita cha Dola za Marekani Milioni 150 nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na namna mataifa yaliyokuwa wenyeji wa michuano kadhaa ya kombe la dunia yalivyopatikana.
Mapema mwezi Desemba manaibu marais wawili wa FIFA Alfredo Hawit na Juan Angel Napout pia walikamatwa kwa tuhma za ufisadi mjini Zurich na kufikisha idadi ya washukiwa kufika 16.
Marekani inaendeleza uchunguzi dhidi ya maafisa hao pamoja na wakurugenzi kadhaa wa makampuni ya matangazo ili kuwafungulia mashtaka.
Kujiuzulu kwa Sepp Blatter
Sepp Blatter ambaye ameongoza FIFA tangu mwaka 1998, alichaguliwa tena kuongoza Shirikisho hilo wakati wa Mkutano mkuu mwezi Mei.
Licha ya ushindi huo, mwezi Juni alitangaza kuwa atajiuzulu katika wadhifa huo na uchaguzi mwingine utafanyika mwezi Februari mwaka 2016.
Uamuzi wa Blatter ulikuja baada ya kupata shinikizo za kujiuzulu kutokana na sakata la ufisadi katika Shirikisho hilo alilokuwa anaongoza.
Wafadhili kama Cocacola,Visa, McDonalds na Budweiser waliongoza shinikizo za kumtaka Blatter alijiuzulu ili kulisafisha Shirikisho hilo na hata kutishia kuondoa ufadhili wake.
Mwezi Septemba, viongozi wa mashtaka nchini Uswizi walivamia Ofisi ya Blatter na kupekuliwa kwa tuhma za ufisadi.
Kamati ya maadili na nidhamu ya FIFA, mwezi Oktoba ilimpiga marufuku ya miezi mitatu Blatter na Naibu wake Mitchel Plattini ambaye pia ni rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya kutojihusisha na maswala ya soka wakati wakichunguzwa.
Blatter anatuhumiwa kutoa malipo ya zaidi ya Dola Milioni 1 nukta 3 yasiyokuwa rasmi kwa Platini, anayosema yalikuwa ni kwa sababu ya ushauri aliutoa kwa Blatter kati ya mwaka 1998 na 2002.
Ripoti zinasema, huenda kamati hiyo ya nidhamu ikawafungia kushiriki katika maswala ya soka kwa muda wa miaka saba.
Blatter ambaye alilazwa hospitalini mwezi Novemba baada ya kukabiliwa na tatizo la msongo wa mawazo, amekanusha kuhusika na ufisadi katika Shirikisho hilo.
Kaimu rais wa FIFA Issa Hayatou
Issa Hayatou, ambaye amekuwa rais wa soka barani Afrika CAF tangu mwaka 1988 alichukua hatamu ya ukaimu wa rais wa FIFA mwezi huu.
Hayatou mwenye umri wa miaka 69, amesema hatawania wadhifa wa urais wa FIFA na atakabidhi madaraka kwa rais mpya pindi tu atakapochaguliwa.
Sheria za FIFA zinamruhusu naibu rais ambaye amekuwa katika wadhifa huo kwa muda mrefu kuchukua wadhifa huo, ikiwa kiti hicho kitasalia wazi.