Wafadhili wakuu wa Shirikisho la soka duniani FIFA, wanamtaka rais Sepp Blatter kujiuzulu mara moja.
Wakiongozwa na kampuni ya Coca-Cola, Visa, Budweiser na McDonald, wafadhili hao wanasisitiza kuwa mabadiliko ya kweli yanaweza kufanyika tu katika Shirikisho hilo ikiwa Blatter ataondoka.
Hatua hii imekuja baada ya viongozi wa Mashtaka nchini Uswizi juma lililopita, kuanza kumchunguza Blatter kwa tuhma za ulaji rushwa.
Blatter mwenye umri wa miaka 79 anatuhumiwa kusaini mkataba ambao ulionekana kutojali maslahi ya FIFA na pia kutoa malipo yasiyokuwa rasmi kwa rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya Mitchel Platini, tuhma ambazo anazikanusha.
Platini ambaye anaonekena kuwa katika mstari wa mbele kuwania urais wa FIFA anasema fedha azizolipwa ni baada ya kazi ya kumshauri Blatter kati ya mwaka 1999 na 2002.
Rais huyo wa FIFA ambaye tayari ametangaza kuwa atajiuzulu baada ya uchaguzi mwingine mwezi Februari mwaka 2016, amesema kwa sasa hawezi kuachia ngazi kwa sababu hatua hiyo haitakuwa kwa maslahi ya Shirikisho hilo.
Viongozi wa sasa wa FIFA na wale wa zamani wamekuwa wakishtumiwa kuhusika na ulaji rushwa akiwemo Katibu Mkuu Jerome Valcke ambaye tayari amesimamishwa kazi.
Makamu wa rais wa zamani wa FIFA Jack Warner, juma hili alipigwa marufu ya maisha ya kutojihusisha na maswala ya soka baada ya kupatikana na makosa ya uvunjifu wa nidhamu.