Shirikisho la mchezo wa soka duniani FIFA, limeagiza Afrika Kusini na Senegal kucheza mchuano mwingine wa kufuzu katika fainali ya kombe la dunia, baada ya refarii aliyechezesha mchezo wa kwanza, Joseph Lamptey kutoka Ghana kupatikana na kosa la kupanga matokeo.
Mwezi Novemba mwaka ulioipita, mataifa haya mawili yalikutana na Afrika Kusini kushinda mabao 2-1 baada ya kupewa penalti iliyolalamikiwa sana na Senegal.
Kosa hili lilisababisha Shirikisho la soka barani Afrika kumfungia kwa miezi mitatu, na baadaye FIFA kumpa adhabu ya kutochezesha soka kipindi chote cha maisha yake.
Hii ni habari njema kwa Senegal ambayo katika kundi D, ni ya tatu kwa alama 5, nyuma ya Cape Verde na Burkina Faso ambazo zina alama sita.
Mechi hiyo itachezwa mwezi Novemba.