Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA Ndugu Gianni Infantino amemshukuru Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace Karia kwa kazi nzuri ya maandalizi ya mkutano wa FIFA wa maendeleo ya mpira (FIFA Football Executive Summit) uliofanyika Februari 22, 2018 Dar es Salaam,Tanzania.
Infantino amesifia mapokezi na maandalizi yaliyofanywa na TFF katika mkutano huo mkubwa uliofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Katika barua yake aliyomuandikia Rais wa TFF Ndugu Karia ,Infantino amesema wameondoka na kumbukumbu zisizosahaulika kuhusu Tanzania ikiwemo urafiki uliojengeka wakati wote waliokuwepo Tanzania.
Aidha Infantino ameshukuru kwa chakula cha usiku kilichoandaliwa kwenye mgahawa wa Cape Town Fish Market lakini pia kwa kukutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Kassim Majaliwa.
Ameshukuru ukarimu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi kwa ujumla huku pia akimshukuru binafsi Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa
Amesema FIFA kwa pamoja wameridhishwa na maandalizi na shughuli zote za mkutano huo na wamepokea mrejesho chanya kutoka kwa wajumbe wote waliohudhuria.
Infantino pia amepeleka salamu za shukrani kwa mjumbe wa kamati ya utendaji CAF Ndugu Leodger Tenga,Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Ndugu Kidao Wilfred na timu yake kwa ukarimu waliouonesha na kujitolea kulikofanikisha mkutano huo.
Katika hatua nyingine Infantino ameridhishwa na utendaji kazi wa TFF tokea Ndugu Karia ameingia madarakani pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Ndugu Kidao akiwataka kuendelea kusimamia mpira katika utaratibu stahiki wenye uwazi kama wanavyofanya sasa.
Tayari msafara wa FIFA umerejea Zurich yalipo Makao Makuu ya Shirikisho hilo.