Shirikisho la soka duniani FIFA, limemruhusu mchezaji wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joe Issama Mpeko kuichezea klabu ya TP Mazembe. Hatua hii inakuja miezi tisa baada ya kusajiliwa na klabu hiyo yenye makao yake mjini Lubumbashi akitokea klabu ya Kabuscorp nchini Angola. Mchezaji huyo ametia saini mkataba wa miaka mitano na Mazembe, na uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukisuburi cheti kutoka FIFA kumruhusu mchezaji wake huyo mpya kuanza kucheza. Mpeko amesema amepokea kwa furaha kubwa habari hiyo na kuahidi kuwa atafanya bidii kuhakikisha kuwa anaisaidia klabu yake. Kocha wa Mazembe Mfaransa Hubert Velud, sasa ana uwezo wa kumchezesha mchezaji huyo katika michuano ya ligi kuu nchini humo lakini pia marudiano ya mchuano wa klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Wydad Casabalanca wiki ijayo mjini Lubumbashi. TP Mazembe ilifungwa ugenini mabao 2 kwa 0 na ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa inafunga zaidi ya mabao 3 ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele ili kutetea taji hili waliloshinda mwaka uliopita.