Shirikisho la soka nchini Gabon, limemteua tena Jorge Costa kuwa kocha wa timu ya taifa kwa muda wa miezi sita.
Costa mwenye umri wa miaka 44 na raia wa Ureno, amekuwa akiifunza Gabon tangu mwaka 2014, na mkataba wake ulimalizika mwisho wa mwezi uliopita.
Kabla ya mkataba wake kumalizika, Costa alikuwa amedhamiria kuiongoza nchi hiyo kucheza katika fainali ya mataifa bingwa barani Afrika itakayofanyika nchini humo mwakani.
Uongozi wa soka nchini humo umesema mkataba huu unaweza kuongezwa au kusitishwa kwa namna ambavyo kocha huyo atakuwa amefanya kazi yake kwa muda huo.
Mbali na Gabon, Costa amewahi pia kuifunza timu ya taifa ya soka ya Cyprus na Romania.
Mara ya kwanza Gabon kucheza katika michuano ya Afrika ilikuwa ni mwaka 1970 na ikarejea tena mwaka 1994.
Mwaka 1996 na 2012 ilifika katika hatua ya robo fainali.
Pamoja na Equatorial Guinea, ilikuwa mwenyeji wa michuano hii mikubwa ya Afrika mwaka 2012.