Klabu ya soka ya Gor Mahia nchini Kenya itamtabulisha rasmi kocha wake mpya, Jose Marcelo Ferreira raia wa Brazil.
Ferreira anayefahamika kwa jina maarufu Zé Maria anatarajiwa kuchukua nafasi ya Frank Nuttall kutoka Scotland aliyejiuzulu na kwenda kuwa kocha msaidizi wa klabu ya Zamalek nchini Misri.
Kazi ya kwanza ya kocha huyu mpya itakuwa mchuano dhidi ya Nairobi City Stars Jumamosi hii jijini Nairobi.
Uongozi wa Gor Mahia unasema umeridhika na Ferreira, na wana imani kuwa atasaidia kuwanyanyua mabingwa hao watetezu wa soka nchini Kenya ambao msimu huu wameanza vibaya.
Kocha huyu mpya aliichezea timu ya taifa ya Brazil mara 25 kwa muda miaka mitano na licha ya kutocheza katika kombe lolote la dunia, aliwakilisha nchi yake katika mashindano ya dunia ya Shirikisho.
Mwaka 2010 alianza rasmi kuwa kocha na kuanza kuifunza klabu ya daraja la chini Group Città di Castello nchini Italia, kabla ya kujiunga na Catanzaro huko Italia na baadaye Ceahlăul FC ya Romania mwaka 2015.
Kuifunza Gor Mahia itakuwa kazi yake ya kwanza barani Afrika.