Klabu ya Gor Mahia ya Kenya siku ya Jumapili, itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, katika mechi ya mwisho ya kundi D, kutafuta alama tatu muhimu, ili kufuzu katika hatua ya robo fainali.
Mechi hiyo itakayochezwa kuanza saa moja jioni saa za Afrika Mashariki, itapigwa katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, kuanzia saa moja usiku saa za Afrika Mashariki.
Mabingwa hao wa soka nchini Kenya, wanakwenda katika mechi hiyo wakiwa na alama sita, na wanahitaji ushindi ili kusonga mbele.
Zamalek ya Misri inayoongoza kundi hilo kwa alama nane, nayo itakuwa nyumbani katika uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria, kuchuna na NA Hussein Dey ya Algeria ambayo ina alama saba.
ZESCO United ya Zambia ambayo tayari imeshaondolewa katika michuano hii, itakuwa mwenyeji wa Asante Katoko ya Ghana katika mechi ya kundi C.
Asante Kotoko ambayo ina alama saba, inahitaji kushinda mechi hiyo ili kufuzu kwa sababu Al-Hilal ya Sudan ambayo ina alama nane inahitaji ushindi nyumbani dhidi ya viongozi wa kundi hilo Nkana ya Zambia ambayo ina alama tisa.
CS Sfaxien ya Tunisia, itakuwa inataka kulinda heshima ya kudni B, baada ya kufuzu katika hatia ya robo fainali katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Enugu Rangers ya Nigeria ambayo inahitaji ushindi ili ifuzu.
Mechi nyingine pia inatarajiwa kuwa kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Salitas ya Burkina Faso, klabu zote zina nafasi ya kufuzu.
Katika mechi za kundi A, AS Otoho ya Congo Brazaville, Hassania Agadir na Raja Casablanca zote za Morocco, zinatafauta nafasi ya kufuzu.
RS Berkane ya Morocco ambayo tayari imeshasonga mbele, itakuwa mjini Agadir kucheza na ndugu zao Hassania Agadir ambayo ina alama tano.
AS Otoho nayo itakuwa mjino Owando kutafuta ushindi dhidi ya Raja Casablanca.