Klabu ya Gor Mahia nchini Kenya imepongezwa kwa kunyakua taji kuu la ligi ya soka nchini humo kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Gor Mahia walitetea taji hilo Jumatano usiku baada ya kuishinda Sony Sugar katika mchuano muhimu kwa kuwafunga bao 1 kwa 0.
Ubingwa huu wa Gor Mahia umekuja mapema kabla ya kumalizika rasmi kwa ligi kuu nchini humo tarehe 7 mwezi Novemba.
Ushindi wa Gor Mahia siku ya Jumatano unamaanisha kuwa hakuna klabu ambayo inaweza kupata alama zaidi ya 66 ilizonazo Gor Mahia hata ikiwa klabu iliyo na nafasi ya pili Ulinzi Stars yenye alama 51 ikiwa hata itashinda mechi zote zinazosalia.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya SportPesa inayosimamia ligi hiyo Jack Oguda amenukuliwa akisema, “Nawapongeza sana wachezaji na uongozi wa klabu ya Gor Mahia kwa ubingwa mliopata msimu huu,”.
“Gor Mahia imeonesha kuwa kufanya bidii, kuwa na nidhamu na kucheza soka safi kunaweza kuifanya kuleta ubingwa,” aliongeza Oguda.
Gor Mahia imeshinda mataji 15 katika historia ya ligi kuu nchini humo.