Watani wa jadi katika ligi kuu ya soka nchini Kenya Gor Mahia na AFC Leopards watamenyana katika mchuano muhimu wa kuwania taji la ligi kuu ya soka nchini humo siku ya Jumapili katika uwanja wa Taifa wa Nyayo jijini Nairobi.
Historia mara nyingi imekuwa ikiipendelea AFC Leopards katika michuano kama hii inayofahamika kama Mashemeji Derby.
Leopards wanaofahamika kwa jina maarufu kama Ingwe, wameshinda mara 28 huku Gor Mahia maarufu kama Kogalo wakishinda mara 26.
Hata hivyo, timu zote mbili zimetoka sare mara 30.
Historia fupi ya mechi tano zilizopita:-
- AFC Leopards 0-3 Gor Mahia
- AFC Leopards 0-2 Gor Mahia
- Gor Mahia 0-1 AFC Leopards
- AFC Leopards 1-1 Gor Mahia.
Gor Mahia inakwenda katika mechi hii ikiwa inaongoza msimamo wa ligi kwa alama 43 baada ya mechi 20, huku AFC Leopards ikiwa katika nafasi ya 12 kwa alama 23 pia baada ya mechi 20.
Wachezaji wa Gor Mahia Meddie Kagere na Timothy Otieno wanaonekana kuwa mwiba kwa beki ya AFC Leopards huku Leopards ikimtegemea Duncan Otieno katika safu yake ya ushambuliaji.