Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la soka barani Afrika CAF, imeitaka klabu ya Gor Mahia nchini Kenya, kulipa faini ya Dola 5,000 baada ya mashabiki wa klabu hiyo kuzua fujo wakati wa mechi ya hatua ya makundi kuwania taji la Shirikisho dhidi ya Rayon Sport kutoka Rwanda.
Mechi hiyo ilichezwa mwezi Agosti kaika uwanja wa Kimataifa wa soka wa Kasarani jijini Nairobi.
Mwenyekiti wa klabu ya Gor Mahia Ambrose Rachier amekiri kupokea barua kutoka CAF na kuwahimiza mashabiki wa klabu hiyo kutorudia tabia hiyo ya kuzua fujo uwanjani.
Baada ya Rayon Sport kufunga bao la pili, mashabiki wa Gor Mahia walianza kurusha chupa uwanjani wakiwalenga wachezaji wa timu pinzani, kwa mujibu wa ripoti ya waamuzi na msimamizi wa mechi hiyo.
Klabu hiyo ina siku tatu, kukataa rufaa lakini uongozi wa klabu hiyo inasema kuwa, bado inathathmini maamuzi ya kuchukua.