Kocha wa klabu ya Zamalek ya Misri Christian Gross amekiri kuwa Gor Mahia ilihitaji kushinda katika mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi ya kuwania taji la Shirikisho.
Gor Mahia ilishinda mechi hiyo kwa mabao 4-2 katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.
Zamalek, ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia mchezaji wake Ibrahim Hassan katika dakika ya saba ya mchuano huo, lakini ilipofika katika dakika ya 25, Jacques Tuyisenge aliisawazishia Gor Mahia.
Ilipofika katika dakika 38, Tuyisenge alifunga bao la pili lakini dakika moja kabla ya muda wa mapumziko, Zamalek ilisawazisha.
Nicholas Kipkirui na Dennis Oliech, ndio waliowapa matumaini mashabiki wa Gor Mahia kwa kufunga mabao mawili ya ziada.
Mabingwa hao wa soka nchini Kenya, wanaongoza kundi la D kwa alama tatu, sawa na Na Hussein Dey ya Algeria ambayo iliishinda Petro de Luanda mabao 2-1.
Mechi nyingine itachezwa tarehe 13, Gor Mahia watakuwa ugenini katika uwanja wa Kimataifa wa Estadio 11 de Novembro jijini Luanda.