Watani wa jadi katika soka la Kenya Gor Mahia na AFC Leopards wanashuka dimbani Jumapili hii katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi kuchukua katika mchuano wa kwanza wa msimu mpya wa ligi kuu ya soka nchini humo mwaka 2016.
Mabingwa watetezi Gor Mahia hadi sasa wamecheza mechi mbili na zote kutoka sare, na sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 2 huku AFC Leopards ikiwa katika nafasi ya nane kwa kwa alama 4 baada ya kushinda mchuano mmoja na mwingine kutoka sare.
Msimu uliopita, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, timu zote zilitoka sare ya bao 1 kwa 1 lakini mchuano wa pili, mechi haikukamilika baada ya mashabiki wa AFC kuleta vujo uwanjani na baadaye Gor Mahia wakazawadiwa ushindi wa mabao 2 kwa 0.
Mara ya kwanza timu hizi kukutana ilikuwa ni mwaka 1968, mchuano ambao Gor Mahia walishinda kwa mabao 2 kwa 1.
AFC, wanapokutana na Gor Mahia huwa ni mchuano unaozua hisia nyingi sana nchini humo na miaka ya hivi karibuni, umepewa jina la Mashemeji Derby au pambano kati ya mashemeji.
Huu utakuwa ni mchuano wa pili kwa kocha mpya wa AFC Leopards Ivan Jacky Minnaert raia wa Ubelgiji ambaye alipewa kibarua cha kuifunza Ingwe, wiki moja iliyopita.
Kocha huyo wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda na Djoliba AC ya Mali, anasema lengo kubwa ni kuiongoza AFC kunyakua ubingwa wa taji la soka msimu huu.
Gor Mahia itacheza mchuano huu ikiwa na mtikisiko wa kuwapoteza wachezaji wake muhimu Michael Olunga na Meddie Kagere na sasa matumaini ya safu ya ushambuliaji inasalia kwa Jacques Tuyisenge raia kutoka Rwanda na Jacob Keli.
Wiki kadhaa zilizopita, kocha wa Kogalo Frank Nutall kutoka Scotland alifutwa kazi baada ya kudai nyongeza ya mshahara lakini shinikizo za mashabiki zikasababisha uongozi wa klabu hiyo kubadilisha uamuzi wao.