Jaribio la baadhi ya viongozi vya vyama vya soka barani Afrika, kutaka kubadilisha kifungu namba 18 cha sheria ya Shirikisho la soka barani Afrika CAF, kinachosema kuwa wanachama wa Kamati kuu ndio wanaoweza kuwania urais wa Shirikisho hilo, halikufanikiwa baada ya kupingwa katika Mkutano Mkuu wa CAF Alhamisi wiki hii jijini Cairo.
Pendekezo hilo liliwasilishwa na rais wa Shirikisho la soka nchini Djibouti, lakini baada ya kupiga kura, ni nchi 16 ndizo zilizounga mkono huku 32 zikipinga pendekezo hilo.
Mataifa matano hayakupiga kura kama Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia na Malawi.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, viongozi wa soka kutoka Rwanda,Sudan Kusini Djibouti, Somalia ,Uganda, Sudan na Tanzania waliunga mkono pendekezo hilo.
Juhudi za rais wa Shirikisho la soka nchini Liberia Musa Bitily kutaka kura kupigwa kwa siri hazikufua dafu na ikalazimika kuwa wajumbe wapige kura kwa kuinua mikono.
Kuanguka kwa pendekezo hilo kuna maanisha kuwa Isaa Hayatou ambaye ameongoza CAF kwa miaka 28, kumpa nafasi ya kuwania tena wadhifa huo mwaka ujao.
Pamoja na hilo, rais wa Shirikisho la solka nchini Ghana Kwesi Nyantakyi na Almamy Kabele Camara kutoka Guinea ndio waliochaguliwa kuingia kwenye Kamati kuu ya FIFA, hatua ambayo inafanya idadi ya wajumbe kutoka Afrika kufikia saba.