Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) iliyokutana Mei 9,2018 Kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Shirikisho Karume,Ilala pamoja na mambo mengine ilipitia mashauri manne yaliyofikishwa kwenye kamati.
Shauri la kwanza lilihusu wachezaji wa Villa Squad Nassoro Makoba,Hamza Habibu na Severine Charles ambao katika mchezo uliowakutanisha Villa Squad na Namungo FC walidaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi Daraja la Pili.
Kamati baada ya kupitia shauri hilo na kupitia ushahidi uliowasilishwa mbele ya kamati imewakuta na hatia kwa kosa la kutaka kumpiga Mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi Daraja la Pili na kutoa adhabu ya kuwafungia mechi tatu na faini ya shilingi laki Tatu kwa kila mmoja,adhabu ambazo zitatumikiwa kwa pamoja kwa mujibu wa kanuni ya 37(12) za ligi Daraja la pili.
Shauri la pili lililosikilizwa na kamati lilimuhusu Katibu wa Mlandizi Queens Rukia Michael ikihusisha mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Premium Lite kati ya Mlandizi Queens na Kigoma Sisterz ambao anadaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi.
Kamati ilipitia shauri hilo na kumkuta na hatia ya kuvunja kanuni ya 41(2) ya Ligi Kuu ya Wanawake kwa kosa la kutaka kumpiga Mwamuzi na ameadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hiyo kwa kufungiwa miezi 2 na faini ya shilingi laki 2 adhabu ambazo zinakwenda kwa pamoja.
Shauri la Tatu lilimuhusu mchezaji wa Transit Camp Hussein Swalehe Nyamandulu ambaye shtaka lake lilikuwa la kutaka kufanya fujo katika benchi la timu ya Toto Africans na kamati imempa onyo kali kwa mujibu wa Ibara ya 10(1) ya kanuni za nidhamu za TFF.
Shauri la Nne lilimuhusu mchezaji wa Mbeya City Ramadhan Malima ambaye aliingia kushangilia goli la Mbeya City katika mchezo wao dhidi ya Young Africans wakati aakiwa tayari ameoneshwa kadi nyekundu.
Kamati imemkuta na hatia na amehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 37(7)(f),amefungiwa mechi 3 na faini ya shilingi Laki Tano lakini kwasababu amekosa mechi moja sasa atatumikia mechi 2 zilizobaki pamoja na onyo kali kwa mujibu wa kanuni ya 10(1) ya kanuni za nidhamu za TFF.
Mashauri mengine kadhaa hayakusikilizwa baada ya kutofika kwa washtakiwa wa mashauri hayo na kamati imeomba wapewe wito wa mwisho ambao kama hawatafika kamati itasikiliza mashauri yao katika upande mmoja na kuyatolea maamuzi.
Ambao hawakufika na hawakutoa taarifa ni George Rast na Shaibu Salim(AFC-Wachezaji),Aristica Cioaba(Azam FC-Kocha),Issa Ngwasho(JKT Mlale-Meneja),Hosea John,Rashid Ally,Hamis Athuman,Casmir Focus(JKT Msange-Wachezaji),Joseph Mkota(JKT Oljoro-Mchezaji),Katregea Kalegea(Mashujaa FC-Mchezaji),Cuthbet Japhet(Toto Africans-Afisa habari),Kelvin Yondan(Young Africans-Mchezaji) wakati Meneja wa Singida United Ibrahim Mohamed yeye alitoa taarifa ya kufiwa na baba yake mzazi.