Mkurugenzi mtendaji wa klabu ya Gor Mahia nchini Kenya Lordvick Aduda ametangaza nia ya kuwania urais wa Shirikisho la soka nchini Kenya FKF.
Aduda amesema ameamua kuwania nafasi hiyo, baada ya shinikizo kutoka kwa wadau mbalimbali wa mchezo wa soka.
Awali, Aduda alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa FKF lakini aliondolewa katika nafasi hiyo mwaka 2012, na amekuwa mkosoaji mkubwa wa uongozi wa sasa ulioingia madarakani mwaka 2016.
“Wadau wa soka wameniambia muda umewadia wa mimi kuchukua hatua za uongozi. Nimekubali wito wao na hivi karibuni nitaweka wazi.” amesema Aduda.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 7 mwezi Desemba.
Kuelekea kwenye Uchaguzi huo, wagombea wengine wameshaanza kujitokeza, wakiwemo Gavana wa zamani wa jimbo la Vihiga, Moses Akaranga na rais wa zamani wa soka nchini humo Sam Nyamweya.
Rais wa sasa Nick Mwendwa ametangaza kuwa atawania tena nafasi hiyo.