Misri, Morocco na Afrika Kusini yanapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Kenya kuandaa michuano ya bara Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN mwaka 2018.
Hatua hii inakuja baada ya Kenya kuonekana kutokuwa tayari miezi sita kabla ya michuano hiyo muhimu inayoandaliwa kila baada ya miaka miwili.
Kenya ilipewa nafasi ya kuandaa michuano hii mwaka 2016, lakini ukosefu wa viwanja inaonekana kuifanya Kenya kukosa nafasi ya kuandaa michuano hii.
Maafisa wa CAF wanatarajiwa kuwasili nchini Kenya wiki mbili zijazo, kuthathmini utayari wa Kenya kuandaa michuano hiyo na kufanya uamuzi wa mwisho.
Hadi sasa Kenya, ina uwanja mmoja tu ambao unaonekana uko tayari kwa michuano hii.
Kanuni za CAF zinaeleza kuwa, mwandaaji wa michuano hii inastahili kuwa na viwanja vinne kama ilivyokuwa mwaka 2016 nchini Rwanda.
Kenya pamoja na miundo mbinu mizuri ya barabara na hoteli, inakosa viwanja.
Uwanja wa Kinoru mjini Meru, Kenyatta mjini Machakos na Nyayo vimekuwa vikikarabatiwa lakini havijakamilika.