Kilimanjaro Queens ya Tanzania bara ndio mabingwa wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA, baada ya kuishinda Harambee Starlets ya Kenya mabao 2-1 katika fainali ya kuwania taji hilo kwa upande wa wanawake.
Mchuano huu kati ya Tanzania na Kenya ulichezwa siku ya Jumanne katika taasisi ya mafunzo ya soka ya Njeru mjini Jinja nchini Uganda.
Mabao ya Kilimanjaro Queens yalifungwa na Mwanahamisi Omari katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo.
Kipindi cha pili, Kenya ilitoka nyuma na kupata bao lao la pekee kupitia Christine Nafula katika kipindi cha pili baada ya kumlalamikia refarii kuhusu bao la pili la Tanzania.
Licha ya kushinda taji hili, mshindi ameondoka mikono mitupu baada ya viongozi wa CECAFA kusema kuwa walikosa wafadhili katika michuano hii.
Kabla ya kuanza kwa mchuano huu wa fainali, Ethiopia na wenyeji Uganda walimenyana katika mchuano wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu mchuano ambao Ethiopia walishinda kwa mabao 4-1.
Baada ya kupoteza mchuano huu, Kenya sasa wanageukia maandalizi ya kufuzu kucheza fainali ya mataifa bingwa barani Afika itakayofanyika nchini Cameroon kati ya mwezi Novemba na Desemba.