Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Himid Mao amekamilisha uhamisho wa kujiunga na klabu ya Petrojet inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.
Ripoti zinasema mchezaji huyo aliyekulia na kuichezea klabu ya Azam ya Tanzania kwa zaidi ya misimu saba amesaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo ya Misri.
Klabu yake ya Azam kupituia ukurasa wake wa Instagram kumtakia kila la kheri Himid Mao ambaye pia ni kiungo wa ulinzi katika timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
Himid Mao alijiunga na Azam akiwa kidato cha kwanza na alikuwemo katika kikosi cha timu hiyo kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2013 na pia kilitwaa ubingwa wa michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2015.
Himid anaongeza idadi ya wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje, wengine ni Abdi Banda anayecheza Baroka FC ya Afrika Kusini, Thomas Ulimwengu anayeitumikia Al Hilal ya Sudan, Simon Msuva anachezea Difaa Al Jadida ya Morocco, Farid Mussa wa Tenerife ya Hispania na Mbwana Samatta ambaye anaichezea KRC Genk ya Ubelgiji.