Kocha wa klabu ya soka ya Majimaji inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara Mika Lonnstrom raia wa Finland, anasema kwa muda ambao amekuwa nchini Tanzania, wachezaji wake wameendelea kuonesha mapenzi makubwa na jitihada kwa mchezo wa soka.
Lonnstrom mwenye umri wa miaka 41 aliisaidia klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya 10 msimu uliopita na kuisaidia Majimaji kutoshushwa daraja.
“Kila siku ninapowaona wachezaji wangu wakija kufanya mazoezi naona mapenzi yao ya dhati ya kuupenda mchezo wa soka,” alisema Lonnstrom.
Kocha huyo ambaye ameiongoza klabu hiyo kwa miezi minne sasa, anaguswa na namna wachezaji hao wanavyojitolea, kuhudhuria mazoezi na kucheza kwa kujitolea hata pale wanapochelewesha malipo.
“Mechi kumi nilizoongoza tulifanikiwa kupata alama 11.Wachezaji walifanya kazi nzuri na sote tulifurahi,”. alisisitiza.
Kabla ya kuja Tanzania, kocha huyo aliwahi kufunza soka nchini Thailand, Maldives na barani Ulaya na anasema anajitahidi kutumia uzoefu alioupata kusaidia soka nchini Tanzania.
“Kuna vipaji hapa Tanzania, kinachostahili kufanyika ni kujengwa kwa vituo vya kukuza vipaji hasa kwa vijana,” alishauri kocha huyo.
Aidha, anashauri elimu kwa waamuzi kutolewa na pia wachezaji wa zamani kujihusisha na mafunzo ya kuwa waamuzi.
“Nafikiri kuna umuhimu wa kurekebisha namna wachezaji wanavyosafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, mara nyingi inachukua muda mrefu na kuwaathiri wachezaji,”.