Kuna hatihati ya Timu ya Taifa ya Zanzibar kuwakosa wachezaji wake muhimu katika michuano ya Kombe la Chalenji wanaocheza Ligi Kuu Bara kutokana na kukabiliwa na majukumu kwenye klabu zao.
Wachezaji hao akiwemo Mwinyi Haji, Matteo Simon na Abdallah Shaibu wa Yanga, Mudathiri Yahya wa Singida United hawajajiunga na Zanzibar Herous ambayo imeshaanza maandalizi ya michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika Nchini Kenya kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 9.
Kocha mkuu wa Zanzibar Hemed Morocco amesema kuna hatihati akawaacha wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sababu viongozi wao wamegoma kuwaruhusu mapema kujiunga na kambi inayofanyika Zanzibar.
“Tunaangalia kama itashindikana tutachukua wachezaji wanaocheza hapahapa Zanzibar kwa sababu hatuwezi kwenda mashindanoni na wachezaji ambao hawajashiriki programu ya mazoezi,”alisema Morocco ambaye aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa Taifa Stars wakati ikinolewa na Charles Boniface Mkwasa.
Wachezaji wengine ambao wanaweza kukosa michuano hiyo ni Seleman Kassim wa Majimaji ya Songea,Kassim Seleman wa Prisons na Abdallah Kheri wa Azam.