Na Victor Abuso,
Mabingwa watetezi na viongozi wa ligi kuu ya soka nchini Kenya siku ya Jumapili walipata ushindi mkubwa katika mchuano wa ligi kuu ya soka nchini humo KPL baada ya kuwachabanga Nakuru All Stars mabao 5 kwa 0 katika mchuano uliochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo jijini Nairobi.
Ushindi huo umeendelea kuiweka kileleni Gor Mahia ambayo kwa sasa ina alama 30 baada ya michuano 12 iliyocheza na alama tisa mbele ya watani wao wa jadi AFC Leopards ambao wana alama 21.
Gor Mahia lilipata bao lake la ufunguzi kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza, kupitia mshambuliaji wake Maddie Kagere.
Mabingwa hao watetezi walianza kwa nguvu katika kipindi cha pili na kupata mabao matatu ndani ya dakika tano ya kipindi hicho kabla ya kupata la tano kabla ya kumalizika kwa mchuano huo.
Kikosi cha Gor Mahia : 23. Bonface Oluoch. 5. Musa Mohamed. ( 79’ Dirkir Glay) 14. Karim Nizigiyimana. 3. Abouba Sibomana. 6. Collins Okoth. 30. Ali Abondo. 18. Harun Shakava. 22. Meddie Kagere. 7.Ronald Omino. ( 68’ Innocent Wafula) 19. Michael Olunga. 10. Khalid Aucho. ( 78’ Eric Ochieng)
Wachezaji wa ziada : 12. David Juma. 9. Timothy Otieno. 25. George Odhiambo. 20. Ernest Wendo.
Kikosi cha Nakuru All Stars: 31.Shayne Indimuli (GK), 4. Teddy Siwa, 20. Amon Muchiri, (54’ Meshack Chakali) 12. Meshack Chakali 15. Frank Balala, 19. Titus Achesa, 8. Hillary Echesa, 34. Elias Kipkemboi , 26. Boniface Akenga, ( 87’ Peter Mwangi)17. Kennedy Owino, (54’ Robert Arot) 10. Carlson Mweresa 16. Geoffrey Maina
Wachezaji wa ziada :1. Martin Lule (GK), 2. William Ochieng, 5.David Seda 9. Lawrence Juma
Katika matokeo mengine katika michuano ya siku ya Jumapili, Sofapaka FC wakiwa mjini Machakos waliwashinda wanasukari Sony Sugar kwa mabao 2 kwa 1 na kwa ushindi huo, wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 21 wakifuatwa na Ulinzi Stars kwa alama 20 baada ya kupata ushindi katika mchuano wake dhidi ya Thika United wa mabao 2 kwa 1.
Wanabenki wa KCB nao wakiwa nyumbani jijini Nairobi waliwashinda mabingwa wa zamani Tusker FC bao 1 kwa 0 na Mathare United wakawafunga Western Stima mabao 2 kwa 1.
Ligi ya KPL inaendelea siku ya Jumatano juma lijalo ambapo Ulinzi Stars watacheza na Mathare United katika uwanja wake wa nyumbani wa Afraha mjini Nakuru, na Bandari FC watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Mbaraki kumenyana na Nakuru All Stars ambao wanashikilia nafasi ya mwisho katika msururu wa ligi hiyo kwa alama tatu.