Kampuni inayosimamia ligi kuu ya soka nchini Kenya KPL, inatarajiwa kubadilisha jina la ligi hiyo baada ya kujiondoa kwa mfadhili Mkuu kampuni ya kubashiri michezo Sportpesa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPL Jack Oguda na Mwenyekiti wa kampuni hiyo Dan Aduda, wameliambia Gazeti la kila siku nchini humo Daily Nation kuwa watatoa mwelekeo mpya hivi karibuni kuhusu ufadhili na jina la ligi hiyo.
Viongozi wa ligi nchini humo wanaendelea kutafuta mfadhili mwingine, kuelekea kuanza kwa msimu mpya hivi karibuni.
Kampuni ya SportPesa imekuwa ikifadhili ligi kuu ya soka tangu mwaka 2015, kwa kima cha Shilingi za nchi hiyo Milioni 80 kila mwaka.
Sportpesa imejiondoa katika ufadhili wa ligi kuu, timu za soka za Gor Mahia na AFC Leopards na mchezo wa raga na bondia baada ya bunge kutunga sheria kuitaka kulipa kodi asilimia 35 ya mapato yote inayopata baada ya kukusanya mapato yake.