Baruani Akilimali wakianza katika kikosi cha kwanza cha Yanga SC dhidi
ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine, Mbeya. Ilikuwa ni mara
ya kwanza kwa Baruani na Paul kuanza katika mchezo wa ligi kuu, lakini
jambo hilo limepoteza mvuto kutokana na mambo muhimu yaliyoonyesha
udhaifu mkubwa wa uongozi wa Yanga msimu huu.
Kupoteza ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara ambao wameutwaa mara nne
katika misimu mitano iliyopita yakiwemo mataji matatu mfululizo-si
jambo la kushangaza, lakini kitendo cha timu hiyo kusafiri kuelekea
Mbeya ikiwa na kikosi cha wachezaji 13 tu-golikipa mmoja ni jambo
ambalo kwa hakika linapaswa kupigwa vita vikali, ni busara kuona
baadhi ya watendaji wa klabu wakijiuzulu wenyewe.
Yanga ilipoteza 2-0 dhidi ya Prisons siku ya Alhamis hii na rasmi
wakavuliwa ubingwa walioushikilia tangu msimu wa 2014/15. Kiungo
mshambuliaji, Emmanuel Martin alianzishwa kama mlinzi wa kushoto,
Matteo Anthony alianzishwa kwa mara ya kwanza msimu huu kama msaidizi
wa Mkomola katika safu ya mashambulizi, na Beno Kakolanya ambaye muda
mwingi wa msimu huu alikuwa nje ya kikosi alianza katika lango.
Haitoshi, Yanga ilikuwa na wachezaji wawili tu katika benchi la akiba-
mshambulizi raia wa Burundi, Amis Tambwe ambaye amecheza mechi yake ya
pili tangu mwaka huu ulipoanza wakati alipoingia kuchukua nafasi ya
Paul, na mchezaji mwingine wa akiba alikuwa kijana Yusuph Suleimani
ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Matteo.
Ilikuwa ni ‘aibu’ kubwa kwa klabu kubwa kama Yanga-mabingwa mara
nyingi wa kihistoria nchini ( mara 27) kuingiza timu uwanjani ikiwa na
wachezaji 13 tu. Hii inamaanisha klabu hiyo haina kikosi ‘hai’ cha
timu ya vijana-kama kingekuwepo waneongezea wachezaji ili kupata
angalu kundi la wachezaji 18 katika mchezo dhidi ya Prisons.
Mbanano wa ratiba sioni kama ni sababu ya Yanga kusafirisha wachezaji
13 Mbeya. Yanga walicheza mechi ya Caf Confederatins Cup Jumapili
iliyopita huko Algers, Algeria. Walisafiri kurejea nchini na wakawa na
masaa 48 tu kabla ya kuwavaa Prisons, Jumapili hii watapaswa kucheza
na Mtibwa Sugar FC katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Jumatano
ijayo watakuwa uwanjani kucheza na Rayon Sports katika michuano ya Caf
Confederations jijini Dar es Salaam.
Ndani ya siku kumi Yanga wanapaswa kucheza mara nne-mechi mbili za Caf
na mbili za ligi kuu, moja nje ya nchi, moja Mbeya ambako ni umbali
unaochukua masaa kumi hadi 12 kwa mwendo wa basi ambao Yanga
wametumia- watatumia tena masaa yasiyopungua tisa ndani ya basi kutoka
Mbeya hadi Morogoro. Kwa Jiografia ya Tanzania ilivyo ni wazi ratiba
hii ni ngumu sana kwao, lakini bado hakuwezi kuleta maana katika
‘hoja’ ya kukosekana wachezaji wa kutosha katika mchezo dhidi ya
Prisons.
Licha ya kwamba walijitahidi mno kuficha ukweli wa kuwepo kwa mgomo
mkubwa wa wachezaji kitendo kilichosababisha kukosekana kwa wachezaji
wengi muhimu wa kikosi cha kwanza katika mchezo waliochapwa 4-0 na USM
Algers wikend iliyopita, mchezo wa Alhamis hii umeonyesha wazi kile
kilichopo klabuni hapo.
Wachezaji wengi wameungana na kuweka mgomo wa kutocheza kutokana na
kutolipwa malimbikizo ya mishahara, posho kwa miezi inayokadiliwa
kufikia minne sasa. Wachezaji wengine bado wanadai klabu malimbikizo
ya pesa zao za usajili.
Algeria kilikwenda kikosi ambacho asilimia 80 ilikuwa ni sawa na
kikosi cha chipili. Manahodha-walinzi wa kati, Nadir Haroub, Kelvin
Yondan na kiungo Mzimbabwe, Thaban Kamusoko wote hawakusafiri jambo
ambalo lilimfanya Andrew Vicent kubeba majukumu hayo, kiungo
Mcongoman, Papy Tshishimbi, mshambulizi Mzambia, Obrey Chirwa, Ibrahim
Ajib, Tambwe, wote hawa hawakusafiri na timu katika mchezo wao wa
kwanza wa kundi la nne katika Confederations Cup.
Uongozi ulitoa sababu zilizile za tangu Februari, 2017 kuwa klabu
inapitia kipindi kigumu kiuchumi. Hilo halikataliwi, lakini jambo la
kushangaza kumekuwa hakuna juhudi zozote za kuhakikisha jambo hilo
linatatuliwa licha ya kuwepo kwa udhamini kutoka kampuni ya SportPesa,
Marcon, Azam Tv, Vodacom, na maji ya Afya.
Vodacom wameweka makadirio ya kima cha chini cha mishahara ya klabu za
Yanga na Simba SC kuwa Tsh.800,000 kila mwezi, SportPesa wanatoa
kiasi kisichopungua milioni 300 za Kitanzania kila baada ya miezi
mitatu kiasi kidogo sana pungufu ya bajeti ya klabu katika mishahara
ya wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine klabuni.
Ucheleweshwaji wa mishahara wakati mwingine ni jambo la kawaida lakini
linapokuwa sugu kwa miezi 15 mfululizo ni hatari na hiki ndicho
kinachowakuta Yanga. Wameenda kuaibika Mbeya kwa sababu uvumilivu wa
wachezaji umefika kiwango cha mwisho. Ongezeko la mgomo ni kubwa zaidi
kwa maana hata wale wachezaji wa kikosi cha vijana nao wamegoma- ndio
maana hawakuwa hata na golikipa wa akiba katika benchi ambalo lilikuwa
na wachezaji wawili tu.
Sikuwa na shaka ya Clement Sanga –kama kaimu mwenyekiti wa klabu
kuiangusha klabu yake. Amekosa mipango ya kuongeza kipato zaidi cha
klabu, amekosa uwezo wa kudhibiti pesa na kupambana na madeni sugu ya
klabu- jambo ambalo sasa limewafanya kubaki na wachezaji 13
tu-watiifu. Nini sasa wanaweza kufanya ili kulinda hadhi ya Yanga
isiendelee kuporokomoka ikiwa na michezo mitano kabla ya kumalizika
kwa ligi kuu na mitano ya Caf Confederations?
Yanga watakwenda katika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya mwenyekiti
iliachwa wazi na Yusuph Manji tangu Mei, 2017 na ni hapo mwelekeo mpya
wa klabu utafahamika ila kwa sasa wanapaswa kupambana kwa kadri ya
uwezo na nguvu zao zote wamalize msimu pasipo matendo zaidi ya aibu
kama tukio la Mbeya kuwa na wachezaji 13 tu.
Wana michezo sita ndani ya wiki tatu zizajo kabla ya kumaliza
msimu-mitano ya vs Mtibwa Sugar, Mwadui FC ( ugenini), Mbao FC, Ruvu
Shooting, Azam FC (nyumbani) na mchezo wa Caf dhidi ya Rayon kutoka
Rwanda (nyumbani) Inasemekana tayari baadhi ya wachezaji wamekubali
kurejea kikosini na wataungana na timu huko Morogoro, lakini wanachama
wa klabu watunze kmbukumbu zote muhimu na kwenda kuwahoji viongozi
waliowapa dhamana katika mkutano mkuu ujao baadae mwezi Juni
talking African football