Ligi kuu ya soka Tanzania bara inaaza kutimua vumbi mwishoni mwa juma hili katika viwanja mbalimbali nchini humo.
Mechi saba zimeratibiwa kupigwa siku ya Jumamosi .
Ndanda FC ya Mtwara watakua wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Nagwanda Sijaona mjini Mtwara.
African Sports watamenyena na mabingwa wa zamani Simba SC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Majimaji wakimenyana na maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Azam FC nao watakuwa nyumbani kupambana na Tanzania Prisons katika uwanja wao wa Chamazi Complex.
Stand United FC itawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga huku Toto Africans wakichuana na Mwadui FC uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Mchuano mwingine muhimu Jumamosi ni kati ya Mbeya City na Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Siku ya Jumapili kutakuwa na mchuano mmoja tu kati ya mabingwa watetezi Yanga na Coastal Union katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Vlabu vya Yanga, Simba na Azam FC ambazo zimeendelea kuchuana katika soka la Tanzania, wametamba kuonesha ubabe katika msimu huu baada ya kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi.