By Fadhili Sizya
Patashika itakuwa jioni hii kwa saa za nchini Tanzania ambapo mechi mbili zitachezwa katika mfululizo wa mashindano ya Ligi Kuu Tanzania bara maarufu TPL.
Wanaoshika usukani wa ligi Yanga watakuwa kibaruani dhidi ya walima alizeti Singida United mechi itakayoanza mapema majira ya saa kumi kamili jioni katika uwanja wa Namfua mkoani Singida huku mechi za mwisho kwa timu hizo wikiendi iliyopita Yanga ikiambulia sare 1-1 dhidi ya wagosi wa kaya Coastal Union nao wapinzani wao wakiibanjua African Lyon 1-0.
Aidha Yanga chini ya kocha Zahera Mwinyi itakuwa na faida kuongezeka kwa mchezaji aliyekuwa majeruhi Hamisi Tambwe hivyo wataunda safu ya ushambuliaji pacha na Heritier Makambo pamoja na Ibrahim Ajibu ambaye ni nahodha wa kikosi hicho cha Jangwani.
Singida wao watakuwa chini ya makocha wao kutoka Serbia kocha mkuu Poadic Dragan na Dusan Momcilovic watakuwa wakisaka ushindi wa pili mfululizo baada ya kufanya vibaya kwenye michuano ya Sportpesa 2019 wakiondoshwa mapema na timu ya Bandari ya Kenya kwa kufungwa 1-0.
Mechi nyingine itakuwa saa moja kamili usiku katika uwanja wa Azam Complex ambapo wenyeji wa dimba hilo Azam fc wataikaribisha timu ngeni katika ligi kuu kutoka mkoani Mwanza klabu ya Alliance Fc.
Alliance inayocheza pasi fupi na kandanda la kuvutia inatarajiwa kuonyesha upinzani kwa matajiri wa Azam ambapo kwenye mechi mwisho waliishinda 2-0 dhidi ya Lipuli huku Azam mechi yao ya mwisho ligi kuu ikiibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Biashara United.
Msimamo wa ligi nafasi nne za juu Yanga anaongoza na alama 54, Azam 47 ,Kmc 35 sawa na klabu ya Simba ambayo itashuka uwanjani kesho kuivaa Mwadui Fc majira ya saa moja kamili usiku katika uwanja wa taifa Dar Es Salaam.