Ligi kuu ya soka nchini Kenya inakamilika mwishoni mwa juma hili baada ya miezi tisa ya kazi ngumu ya kusaka ubingwa.
Ligi hiyo ya SportPesa inakamilika huku mabingwa watetezi Gor Mahia wakiwa tayari wameshanyakua ubingwa wa msimu huu.
Vlabu vyote 16 vitashuka dimbani kuanza saa tisa mchana kukamilisha mzunguko wa 30 wa ligi hiyo msimu huu.
Mabingwa hao ambao wameshinda taji hili misimu mitatu mfululizo watakabidhwa kombe siku ya Jumapili katika uwanja wa taifa wa Nyayo jijini Nairobi.
Gor Mahia ambao hawajapoteza mchuano wowote msimu huu watacheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Muhoroni Youth ikiwa itapata ushindi au kutoka sare itaingia katika vitabu vya kihistoria kwa kunyakua ubingwa bila kufungwa.
Hadi sasa klabu ya Nakuru All Stars imeshushwa daraja na kati ya KCB na Nairobi City Stars klabu moja pia itashushwa daraja.
Klabu ya AFC Leopards itacheza mchuano wake wa mwisho dhidi ya Tusker katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani bila ya kocha wake Zdravko Logarusic aliyeachana na klabu hiyo mapema juma hili kutokana na matatizo ya kifedha lakini pia Tusker itakosa huduma za mkufunzi wao Francis Kimanzi aliyejiuzulu wiki tatu zilizopita.
Mfungaji bora katika ligi hiyo pia atafahamika siku hiyo kwa sababu hadi sasa mshambuliaji wa Tusker FC Jesse Were ana mabao 20 huku mpinzani wake wa karibu Michael Olunga wa Gor Mahia akiwa na mabao 18.
Mabingwa Gor Mahia mbali na kombe watakabidhwa pia Kitika cha Shilingi za Kenya Milioni 4 nukta 5.
Ratiba Kamili (Mechi zote kuanza saa 9 mchana):
Nakuru All Stars v Ushuru (Oserian Stadium)
Gor Mahia v Muhoroni Youth (Nyayo Stadium)
City Stars v SonySugar (City Stadium)
Chemelil Sugar v Mathare United (Chemelil Sugar Sports Complex)
Western Stima v KCB (Moi Stadium)
Sofapaka v Thika United (Ruaraka ground)
AFC Leopards v Tusker (Kasarani Stadium)
Ulinzi Stars v Bandari (Afraha Stadium)