Msimu mpya wa ligi kuu ya soka nchini Uganda ilianza siku ya Ijumaa wiki hii, huku ile ya Tanzania bara ikifungua milango yake siku ya Jumamosi.
Nchini Uganda, mechi nane zilichezwa katika siku ya kwanza katika viwanja mbalimbali nchini humo.
Mabingwa watatezi KCCA FC kutoka jijini Kampala wakiwa nyumbani, walianza vema baada ya kuishinda Hippos FC kutoka mji wa Jinja kwa ushindi wa mabao 2-1 katika uwanja wa Philipp Omondi.
Mabao ya KCCA yalitiwa kimyani na washambuliaji Joseph Ochaya na Geofrey Sserunkuma huku Hippos wakipata bao lao kupitia mchezaji Viane Sekajugo.
Matokeo kamili:
KCCA 2-1 JMC Hippos
Express FC 2-1 Lweza FC
SC Vipers 1-1 Bright Stars FC
Police FC 0-0 SC Villa Jogoo
The Saints FC 0-0 SC Villa Jogoo
The Saints FC 0-0 Sadolin
BUL FC 0-0 Proline FC
Kirinya Jinha SS 0-0 URA FC
Onduparaka FC 0-0 Soana FC
Ligi hii itarejelewa tena siku ya Jumanne Agosti 23 kwa vlabu vyote kushuka dimbani.
Nchini Tanzania, baada ya Azam FC kuwashinda mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka nchini humo Yanga FC, katika fainali ya taji la ngao ya hisani wiki hii, msimu mpya wa ligi kuu unaanza siku ya Jumamosi.
Yanga FC yenye makao yake jijini Dar es salaam itasubiri hadi Agosti 31, kuanza kutetea taji lake dhidi ya African Lyon kwa sababu inajiandaa kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumaliza ratiba yake ya kuwania taji la Shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe siku ya Jumanne wiki ijayo mjini Lubumbashi.
Mechi tano zimepangwa kupigwa siku ya Jumamosi katika viwanja mbalimbali nchini humo.
Simba SC itaikaribisha Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni wakati Azam itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam FC ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji.
Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga sawa na Mtibwa Sugar itakayoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Manungu uliuoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro wakati Prisons ya Mbeya itasafiri hadi Uwanja wa Majimaji ya Songea kucheza na Majimaji FC .
Jumapili Agosti 21 2016-Kagera Sugra vs Mbeya City.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeonya timu kuchezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.