Maafisa wawili wa juu wa Shirikisho la soka duniani FIFA, wamekamatwa mjini Zurich nchini Uswizi kwa tuhma za ufisadi.
Hatua hii inakuja wakati huu viongozi wa Kamati Kuu ya utendaji ya FIFA inapokutana kuyapigia kura mabadiliko muhimu ya namna ya kusimamia vema mchezo wa soka .
Uongozi wa FIFA unasema ulikuwa na taarifa kutoka kwa idara ya sheria na haki nchini Marekani kuhusu kukamatwa kwa mawili hao wanaotuhumiwa kwa wizi wa Mamilioni ya Dolla za Shirikisho hilo.
FIFA inasema itaendelea kushirikiana na wachunguzi wa Marekani pamoja na wale wa Uswizi kuwafungulia mashtaka maafisa wa Shirikisho hilo wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi.
Maafissa hao kwa sasa wanashikiliwa wakisubiri kusafirishwa nchini Marekani kwa mahojiano zaidi.
Viongozi wa mashtaka wanasema watayaweka wazi majina ya maafisa hao waliokamatwa baadaye siku ya Alhamisi.
Mwezi wa tano mwaka huu, maafisa wengine saba wa FIFA walikamatwa katika hoteli hiyo kwa tuhma za ufisadi, madai ambayo wanaendelea kuyakanusha.
Sepp Blatter rais wa FIFA na naibu wake Mitchel Platinni wamepingwa marufuku kushiriki katika maswala ya soka kwa muda wa miezi mitatu kwa tuhma za ufisadi ambazo wamezikanusha.
Uchaguzi mpya wa rais wa FIFA umeratibiwa kufanyika baadaye mwezi Februari mwaka ujao wa 2016.
Shirikisho hilo kwa sasa linaongozwa na Issa Hayatoue rais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF.