Madagascar, Senegal , Tunisia , Misri yamekuwa mataifa ya kwanza kufuzu katika fainali za mataifa bingwa barani Afrika AFCON, mwaka ujao nchini Cameroon.
Ni furaha kubwa kwa Madagascar ambayo imefuzu kwa mara ya kwanza baada ya kupata ushindi muhimu dhidi ya Equitorial Guinea kwa kuifunga bao 1-0,lililotiwa kimyani na Njiva Rakotoharimalala.
Ndoto ya Madagascar imetimia baada ya kujaribu kufuzu katika mashindano haya mara 18 bila mafanikio.
Kuelekea fainali hizi, Kocha Nicolas Dupuis ambaye ni Mfaransa, aliwatumia wachezaji wengi wanaocheza soka ugenini wakiwemo wanne wanaocheza Ufaransa na wengine Ubelgiji, Misri, Saudi Arabia na Algeria.
Senegal nayo iliishinda Sudan 1-0 na kujihakikisha nafasi ya kwenda nchini Cameroon, mechi iliyochezwa jijini Khatroum siku ya Jumanne.
Misri ambao wanashikilia rekodi ya kushinda taji hili mara saba, walipata matokeo mazuri baada ya kuifunga Eswatini mabao 2-0 mjini Manzini, huku Tunisia ikiilemea Niger kwa ushindi wa mabao 2-1 jijini Niamey.
Baada ya mechi nne, Tunisia inaongoza kundi la J kwa alama 12 huku Misri ikiwa ya pili kwa alama 9. Eswatini na Niger, zina alama moja.
Timu nyingine ambayo imefuzu ni Cameroon ambayo inacheza mechi za kujiandaa kwa sababu tayari imefuzu kwa sababu wao ni wenyeji.
Mataifa mengine ambayo yapo katika nafasi nzuri ya kufuzu ni Kenya na Ghana kutoka kundi F. Matumaini ya Harambee Stars yalionekana mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kuishinda Ethiopia mabao 3-0 jijini Nairobi.
Hatima ya Sierra Leone haijawa wazi, baada ya kufungiwa na Shirikisho la soka duniani FIFA, kwa sababu serikali iliingilia masuala ya usimamizi wa soka nchini humo kinyume na kanuni .
Uganda nayo inaelekea kufuzu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Lesotho jinini Maseru. Mechi ya kwanza, ilipata ushindi wa mabao 3-0 jijini Kampala na inaongoza kundi la L kwa alama 10, ikifuatwa na Tanzania ambayo ina alama 5 baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde ambayo baada ya mechi nne, ina alama nne.