Sherehe zimeendelea leo Jumatatu katika mji wa Lubumbashi na kwingineko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya klabu ya TP Mazembe kunyakua taji la klabu bingwa barani Afrika mwishoni mwa juma lililopita.
Mchambuzi na mwanahabari wa michezo Pacheco Kavundama ameimbia soka25east.com kuwa mashabiki bado wanakunywa pombe kufurahia ushindi huo.
“Ndio sherehe zaendelea sana,kuna watu wangali natumia kinyaji ju furaha,” alisisitiza Kavundama kwa Kiswahili kinachozungumzwa nchini DRC.
TP Mazembe iliishinda USM Alger ya Algeria katika awamu zote mbili za fainali, ugenini na nyumbani kwa jumla ya mabao 4 kwa 1.
Majuma mawili yaliyopita, Mazembe inayomilikiwa na tajiri Moise Katumbi Chapwe iliishinda USM Alger mabao 2 kwa 1 na Jumapili iliyopita ikapata ushindi muhimu wa mabao 2 kwa 0, mabao yaliyotiwa kimyani na Mbwana Sammata kutoka Tanzania na Roger Assale kutoka Cote Dvoire.
TP Mazembe ambayo sasa imeshinda taji hili mara tano katika historia ya michezo hii, inajiunga na Zamalek ya Misri kuwa miongoni mwa vlabu vilivyopata mafanikio katika mashindano haya ikiwemo Al Ahly pia kutoka Misri ambayo imeshinda taji hili mara nane.
Aidha, Mazembe inakuwa klabu ya tatu barani Afrika kushinda fainali ya taji hili ugenini na nyumbani baada ya Hafia ya Guinea na Hearts of Oak ya Ghana.
Wafungaji bora ni Bakri Al-Madina kutoka klabu ya Al-Merrikh na Mbwana Samatta wote wana mabao 7.
Baada ya ubingwa huu, vijana hao sasa wanajiandaa kushiriki katika fainali za kombe la dunia baina ya vilabu mwezi Desemba nchini Japan.